Rais wa serikali ya Wanafunzi Madaktari wa Chuo kikuu cha Bugando (CUHASSO) Musa Leonard Mdede (Katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa tamko kwa niaba ya wanachuo kuiomba Serikali kutoa udhamini wa ada kwa asilimia 100 kwani wanafunzi wengi wanashindwa kumaliza masomo yao kutokana na kujikita kwenye shughuli za usakaji pesa kwa ajili ya malipo, nazo ada zikiendelea kupanda kila msimu huku Serikali ikiendelea kutoa ufadhili kwa asilimia ileile.
"Tunaiomba Serikali kuongeza kiwango cha ufadhili ili wanafunzi au vijana walio na nia ya kusoma fani ya udaktari wakiwa wanalenga kuokoa maisha ya watanzania watimize ndoto zao. Tunatambua kuwa nchi yetu ina upungufu wa asilimia 60 ya madaktari wa sekta ya afya"
"Na kwa takwimu daktari mmoja anahudumia zaidi ya wagonjwa 33,000 kutokana na idadi ya watanzania wote, sasa kuendelea kuwa na vijana wanaoshindwa kuendelea na masomo ya sekta ya afya kwa sababu ya kukosa karo, nikurudi nyuma na kamwe malengo hayatotimia" Alisema Musa Leonard Mdede
Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi Madaktari wa Chuo cha Bugando (CUHASSO) Atukuzwe Mordekai Gwihangwe (katikati) akitoa ufafanuzi jinsi ada kubwa inayotozwa kwa wanafunzi inavyokwamisha malengo ya wanafunzi wa sekta ya Afya nchini hali inayopelekea serikali kukosa wataalamu wa kutosha. Kushoto ni Rais wa CUHASSO Musa Leonard Mdede na kushoto ni Benjamin Thomas